پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Kutayarisha Chakula

Kutayarisha Chakula

Wajibu mwingine muhimu sana wa mama wa nyumba ni kutayarisha chakula cha familia yake. Mama mwenye nyumba mzuri, pia ni mpishi mzuri ambaye anaweza kutayarisha chakula kitamu kwa fedha kidogo, ambapo mama wa nyumba mbaya hupika chakula kibaya kwa kutumia viungo vya gharama kubwa. Chakula kitamu ni njia ya kumvutia mume wako aelekee kwako. Mwanaume ambaye mke wake hupika vizuri, hafurahii zaidi kwenda kula nje.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Mwanamke bora zaidi miongoni mwa wanawake zenu ni yule anayejipuliza manukato, hutayarisha chakula kwa ustadi na hadekezi tabia ya kutumia fedha kwa israfu. Mwanamke wa aina hii ni kundi la wafanyakazi wa Mwenyezi Mungu na mtu anayefanya kazi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kamwe hatapatwa na majuto au kushindwa.”

Haiwezekani kuandika orodha ya aina za mapishi, lakini vipo vitabu vingi vizuri kuhusu somo hili ambavyo vinaweza kupatikana na kutumiwa kupika chakula kitamu.

Lakini mambo machache ya kukumbuka: Nia ya kula chakula si kujaza tumbo lakini pia kwamba hugawia mwili lishe yote inayohitajika kuendeleza kazi yake. lishe muhimu inayohitajiwa na mwili ipo kwenye nyama, matunda, mboga na nafaka na inaweza kuainishwa katika makundi sita: Maji.

Madini; kama vile kalisi/chokaa,fosforasi, chuma, shaba na kadhalika. Vitu vyenye wanga yaani kabohaidreti. Mafuta. Protini. Vitamini kama A, B, C, D, E na K.

Sehemu kubwa ya uzito wa mtu ni maji. Maji huyeyusha chakula kigumu ili kiwe tayari kufyonzwa na utumbo mdogo. Maji pia hurekebisha joto la mwili.

Madini ni muhimu kwa kukua mifupa, meno, na kurekebisha utendaji wa misuli.

Kabohairdate hutengeneza nguvu na joto.

Protini husaidia mabadiliko ya seli mpya kushika nafasi ya zilizozeeka au zilizokufa na kusababisha kukua kwa mwili.

Vitamini pia ni muhimu kwa kukuza na kuimarisha mifupa, kurekebisha majibizo ya kemikali kwenye mwili na ni muhimu kudumisha mfumo mzuri wa neva nzuri.

Kila kitu kilichotajwa hapo juu ni muhimu kwa mwili. Utapiamlo husababisha maradhi mengi na unaweza kuua. Ubora wa chakula ni muhimu na upo uhusiano wa uwiano wa urefu wa kipindi cha maisha ya mtu, furaha na huzuni, uzuri na ubaya na neva zenye afya au maradhi ya akili.

Tunaonekana tulivyo kufuatana na tulicho kula. Kama mtu anafuatilia chakula chake na kujali mazoea ya ulaji wake, hatapata maradhi mara kwa mara. Si busara kula chakula kitamu bila kutafakari ubora wake. Mara afya ya mtu inapoharibika kwa sababu ya chakula kibaya, lazima atafute daktari wa kumtibu, lakini bahati mbaya mwili wa binadamu kamwe hautarudi katika afya yake ya ya mwanzo.

Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alisema: “Tumbo ni kituo cha maradhi yote.”

Kwa kuwa chaguo la chakula ni jukumu la wanawake, kwa hiyo, wanao wajibu wa afya ya familia. Uzembe mdogo sana kwa upande wa mwanamke, utaiweka afya ya familia yote katika hali ya kushambuliwa na maradhi mengi.

Kwa hiyo, mama mwenye nyumba, pamoja na yeye kuwa mpishi mzuri, lazima awe na uwezo wa kutambua ubora wa chakula.

Kwanza: Atalazimika kutayarisha chakula ambacho kina lishe muhimu kwa mwili wa binadamu kufanya kazi inavyostahili. Mtume (s.a.w) wa Mwenyezi Mungu alisema:

Wajibu wa mwanamke kwa mume wake ni kuwasha taa ndani ya nyumba na kutayarisha chakula kizuri na kinachofaa.”

Mwanamke alimuuliza Mtume (s.a.w) wa Mwenyezi Mungu: “Ni thawabu nzuri kiasi gani zinazomngoja mwanamke anayetimiza wajibu wake kwa mume wake?” Mtume (s.a.w) alisema: “Kwa kila shughuli anayoifanya ambayo inahusu mambo ya familia, Mwenyezi Mungu humtazama kwa jicho la wema, na yeyote anayefurahia neema za Mwenyezi Mungu hatateswa.”

Pili: Mahitaji ya chakula ya watu hutofautiana. Umri, saizi ya mwili na vipengele vingine hubainisha kiwango cha mahitaji yetu ya lishe. Mathalani mtoto ambaye anakua huhitaji kalisi/chokaa zaidi ikilinganishwa na mahitaji ya madini ya aina hiyo ya mtu mwenye umri wa utu mzima. Vijana wanahitaji lishe yenye kuongeza nguvu zaidi kwa sababu wana shughuli nyingi zaidi.

Kazi ya mtu pia ni kipengele kinachobainisha aina ya chakula ambacho mtu anatakiwa kula. Mathalani, anayefanya kazi ngumu anahitaji chakula cha mafuta zaidi, sukari na wanga kwa sababu anashughulika sana.

Hali ya hewa ni kipengele kingine. Mahitaji ya lishe yetu kutofautiana kufuatana na msimu wa joto na baridi. Pia mtu mgonjwa chakula chake hutofautiana na kile cha mtu mwenye afya njema. Mpishi mzuri lazima akumbuke mambo yote haya.

Tatu: Ni kweli kwamba mtu anapofika umri wa miaka arubaini na zaidi, upo uwezekano wa kunenepa. Labda baadhi ya watu huona kuwa na kitambi ni dalili ya afya njema, lakini fikra hiyo si sahihi. Kuota kitambi ni ugonjwa ambao unaweza kusababisha athari mbaya sana kwenye moyo, shinikizo la damu, mafigo, kibofu cha nyongo, ini, na huweza kusababisha maumivu kifuani na kisukari.

Takwimu kutoka kwenye vyanzo vya tiba na kampuni za bima hushauri kwamba watu wembamba huishi kwa muda mrefu kuliko wanene.

Baada ya miaka arobanini, mtu hupunguza shughuli kwa hiyo anahitaji mafuta, sukari na wanga kidogo. Kalori hazigeuzwi kuwa nishati kwa wingi kama mwanzo kwa hiyo huchangia mwili kunenepa. Kwa hiyo ni bora kupunguza kula vitu hivi.

Mwanamke anayejali afya ya mume wake anatakiwa amtengenezee lishe maalum ili asinenepe. Lazima apunguze kula vitu vitamu, vinono na, lakini azidishe kula mayai, ini nyama ya kuku, nyama isiyo na mafuta, samaki na jibini. Bidhaa za maziwa pia zinazo manufaa.

Akiruhusiwa na daktari mtu mwenye uzito mkubwa anatakiwa kula matunda na mboga kwa wingi.

Kama umechoshwa na mume wako, kama unataka kuwa mjane, au kama unataka kumuua mume wako bila hatari ya kushtakiwa na polisi - basi unatakiwa kufanya jambo dogo tu. Mpe chakula kingi kitamu na cha kunenepesha. Mhimize ale mkate, wali na keki kwa wingi iwezekanavyo. Matokeo yake utamwondoa na si tu kwamba utakuwa mjane bali atakuwa amekushukuru kwa kumlisha vyakula vyote hivi vitamu.

Unaweza kushauri kwamba utaratibu wa aina hii unaweza kutekelezwa na watu matajiri ambao wanaweza kununua aina yoyote ya chakula wanachotaka. Unaweza kufikiria haiwezekani kwa watu wasio matajiri kuweka utaratibu kama huu.

Lakini mtu asisahau kwamba manufaa yote ya lishe yamejificha kwenye vyakula rahisi vya kawaida. Mwanamke ambaye amejifunza kuhusu mapishi atakwambia kwamba mtu anaweza mahitaji yote ya lishe ya mwili kutoka kwenye vyakula kama vile matunda, nafaka, mboga na bidhaa za maziwa.

Mtu anaweza kupika mlo kwa viambato hivi ambavyo vinaafikiana na elimusiha, afya na bila gharama.