پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Usafi

Usafi

Mojawapo ya wajibu muhimu wa mama wa nyumbani ni kudumisha usafi ndani ya nyumba. Usafi ni ufunguo kwa elimusiha na afya. Huzuia maradhi mengi na huwavutia watu wa familia. Ni chanzo cha heshima kwa familia.

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Dini ya Uislamu msingi wake ni usafi.”

Mtume (s.a.w) pia alisema: “Uislamu ni safi kabisa, kwa hiyo lazima ufanye jitihada kuwa safi kwa sababu ni watu walio safi tu ndio watakaoingia Peponi.”

Kila mara iweke nyumba yenu katika hali ya usafi na kupanga vizuri. Futa vumbi mara moja kila siku na ondoa madoa yote na uchafu wote kutoka kwenye kuta, milango, madirisha, fenicha na vitu vingine. Weka taka kwenye pipa la taka lenye mfuniko, liweke mbali na vyumba vingine na jiko. Takataka zikijaa kwenye pipa la taka zimwage panapostahili. Kila mara usiweke taka mbele ya nyumba yenu. Usiwaruhusu watoto wenu wakojoe kwenye bustani au ua, na wakifanya hivyo, safisha sehemu hiyo kwa maji haraka. Usilundike vyombo vichafu. Vioshe haraka iwezekanavyo. Usisahau kwamba virusi vya hatari hukua kwenye uchafu na vinaweza kuwa vya hatari kwako na familia yako. Osha vyombo kwa maji safi, na baada ya hapo viweke kwenye sehemu iliyo safi. Kusanya nguo zote chafu, hususan nepi za watoto kutoka kwenye vyumba vyote na jiko na uzifue haraka iwezekanavyo.

Weka nguo za familia zote hususan nguo za ndani, safi na nadhifu. Osha nyama na mboga za majani na mchanganyiko wote wa chakula kabla ya kupika. Osha matunda yote kabla ya kula kwa sababu baadhi yao hupuliziwa sumu ya kuua wadudu.

Nawa mikono kabla na baada ya kula na wafundishe watoto wenu kufanya hivyo. Baada ya kula chakula nawa mikono na modomo. Kama inawezekena piga mswaki meno kila baada ya mlo. Kupiga mswaki ni jambo muhimu, angalau mara moja kwa siku, ni vema zaidi kabla ya kulala.

Kata kucha zako mara moja kwa wiki. Kucha ndefu si elimusiha, kwa sababu virusi vinaweza kuishi kwenye kucha ndefu. Oga, angalau mara moja kwa wiki au kama inawezekana kila baada ya siku moja.

Lazima unyoe nywele kwenye kwapa pamoja na sehemu zingine. Nywele zilizojificha kwenye mwili ni mahali panapoweza kuishi virusi vinavyokua. Usiruhusu nzi watue kwenye chakula kwa sababu nzi ni wasafirishaji wa vijiumbe hatari vya maradhi.

Dini Tukufu ya Uislamu inapendekeza kwa kusisitiza watu waangalie usafi. Imam Sadiq (a.s) alisema:

“Mwenyezi Mungu Mweza wa yote hupenda mapambo, sura ya kuvutia na hapendezewi kuona hali ya kujifanya maskini. Hupenda kuona athari za neema zake kwa mja wake, yaani, kumuona akiwa safi, nadhifu na kutumia manukato, kuremba nyumba yake, kupangusa vumbi kwenye mazingira ya nyumba yake kuwasha taa kabla ya jua kuchwa kwa sababu kitendo hiki huondoa umasikini nyumbani na kuongeza riziki.”

Mtume (s.a.w) alisema: “Mtu mchafu ni mja mbaya (kwa Mwenyezi Mungu)”

Imamu Saiq (a.s) alisema: “Iweke nyumba yako katika hali ya usafi na kuondoa utando wa buibui kwa sababu utando wa buibui husababisha umasikini.”

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Usiache uchafu ndani ya nyumba wakati wa usiku kwa sababu shetani huishi humo (yaani, kwenye uchafu na najisi).”

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Nguo za mtu lazima ziwe safi kila mara.” 101

Akiongezea, Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alisema: Usiache nguo yenye mafuta ndani ya nyumba, kwa sababu shetani hufanya makazi yake hapo.”

Imam Sadiq (a.s) alisema: “Kuosha vyombo na kusafisha mazingira ya nyumba huongeza riziki.”

Imam Sadiq (a.s) pia alisema: “Usiache vyombo bila kuvifunika, vinginevyo shetani huvitemea mate na kuvitumia.”

Kwa kuongezea Imam Sadiq (a.s) alisema: “Matunda hupulizwa madawa yenye sumu, kwa hiyo, yakosheni kabla ya kula.”

Imam Kazim (a.s) alisema: “Kuoga kila baada ya siku moja humnenepesha mtu.”

Mtume (s.a.w) wa Mwenyezi Mungu alisema: “Usiache uchafu nyuma ya mlango wa mbele wa nyumba kwa sababu shetani hufanya masikani hapo.”

Mtume (s.a.w.w) wa Mwenyezi Mungu pia alisema; Kama ingekuwa si jambo la usumbufu kwa wafuasi wangu, ningewaagiza kupiga mswaki meno yao kila wanapochukua wudhu kwa ajili ya sala (yaani mara tano kwa siku).”

Imamu Sadiq (a.s) alisema: “Kukata kucha kila siku ya Ijumaa huzuia maambukizi ya ukoma, kichaa na kupofuka macho.” 109 Imesimuliwa kwamba shetani hulala usingizi chini ya kucha ndefu.”

Imamu Ali (a.s) alisema: “Kunawa mikono kabla ya kuanza kula chakula, hurefusha maisha, huzuia nguo za mtu kuchafuka na kung’arisha macho ya mtu.”