پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Endapo Mnatakiwa Kuishi Nje Ya Mji Wa Nyumbani

Endapo Mnatakiwa Kuishi Nje Ya Mji Wa Nyumbani

Mtu anaweza kutakiwa kuishi nje ya mji wa nyumbani kwake. Mume wako anaweza kuwa anafanya kazi kwenye sekta binafsi au ya umma, na akahamishwa na kupelekwa kwenye mji mwingine. Watu wengine huishi hivi ama kwa muda au moja kwa moja. Wanaume wanalazimika kuvumilia hali hii lakini wanawake wengine hupenda kuwa karibu na wazazi wao na ndugu zao.

Wanawake hawa wamezoea mitaa, kuta ndefu na mazingira ya mahali walipozaliwa. Baada ya kuhama huanza kuwalaumu waume zao na kulalamika:

“Kwa nini niishi mbali na nyumbani? Hadi lini nitakuwa mbali na nyumbani, na wazazi wangu? Sina mtu mahali hapa. Umenileta wapi hapa? Siwezi kuishi hapa; Kwa hiyo fikiria namna ya kutatua tatizo hili!”

Wanawake hawa hawatakiwi kuwatibua waume zao namna hii. Wanawake hawa ni dhaifu sana kiakili hivyo kwamba wanadhani mahali waliko zaliwa ndizo sehemu nzuri zaidi kuishi. Wanafikiri kwamba hawawezi kufurahia maisha mahali pengine.

Binadamu haridhishwi hata na sayari yake, kwa hiyo, ameanza kwenda kwenye sayari nyingine. Lakini mtu anamuona mwanamke ambaye hafikirii, wakati ujao hata kidogo hivyo kwamba hayupo tayari kuishi umbali wa maili chache kutoka mji wa nyumbani kwake. Yeye anafikiri; “Kwa nini niwaache marafiki zangu na ndugu zangu wote niende ugenini?” Inakuwa kama vile mwanamke huyu hajiamini vya kutosha kuweza kupata marafiki wapya mahali pengine mbali na alikozaliwa.

Mpendwa mama! Uwe na busara na mwenye kujitolea. Usiwe mbinafsi. Sasa kazi ya mume wako imekuondosha kutoka kwenye mji wa nyumbani kwako, usimsababishie usumbufu. Kama yeye ni mfanyi kazi serikalini, ameamuriwa kuondoka kwenda kwenye kazi na kama anayo biashara binafsi, basi kwa hakika ni kwa manufaa yake mwenyewe kuishi mahali pengine.

Endapo mume wako anakutaarifu kwamba anakwenda kuishi sehemu nyingine, unatakiwa kukubali mara moja. Unatakiwa kumsaidia kufunga mizigo na kwenda mahali pa ugenini ambako lazima ujaribu kuhisi upo nyumbani. Panga maisha yako hapo ambapo ndio nyumbani kwako na ujirekebishe ili upazoee. Kwa kuwa wewe ni mgeni katika sehemu hii na labda huna mazoea na tabia za wakazi wa hapo, uwe na tahadhari nao. Baada ya muda, kwa msaada wa usimamizi wa mume wako, jaribu kupata marafiki kutoka kwa wanawake safi na wakuaminika.

Kila sehemu inayo sifa zake. Unaweza kujipumzisha kwa kuona sehemu za kuvutia na kutembelea majengo ya zamani.

Lazima muweke familia pamoja na umtie moyo mume wako katika kazi yake. Baada ya muda utazoea nyumba yako mpya na inawezekana hata ukapapenda zaidi kuliko ulikotoka. Unaweza ukaona kwamba marafiki zako wapya ni bora zaidi kuliko wa zamani.

Endapo hiyo sehemu mpya itakosa starehe za mji wa zamani, basi zoea maisha mapya na tafuta sifa zake. Endapo hakuna huduma kama vile umeme, basi mazingira yenu yanaweza kuwa na hali ya hewa nzuri zaidi na mnaweza kupata vyakula vibichi na vyenye ubora wa kiwango cha juu. Kama hakuna barabara nzuri basi hamtavuta hewa yenye sumu kutoka kwenye moshi wa magari na hamtasumbuliwa na kelele za watu na magari.

Wafikirie wanaume na wanawake wanaoishi vijijini kwa furaha kwenye nyumba za matofali ya udongo na hawatajali kwa vyovyote vile starehe za jiji na nyumba zao nzuri zifananazo na kasri. Fikiria mahitaji yao na yale wanayoyakosa. Kama unaweza kuwasaidia, basi usisite na mtie moyo mume wako kuwa na msaada kwao. Kama wewe unayo busara na unafanya kazi yako, basi utaishi kwa raha kwenye sehemu hiyo ya ugenini. Unaweza kuwa na msaada kwa maendeleo ua mume wako. Kwa njia hii utajulikana kama mke unayeheshimiwa na kujitoa katika mambo mema. Utapendwa na mume wako na utakuwa maarufu miongoni mwa watu. Zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu ataridhika na wewe.