پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Kubali Uongozi Wake

Kubali Uongozi Wake

Kila taasisi, kiwanda na shirika huhitaji meneja muajibikaji. Kwenye kila kitengo cha jamii na shirika, ushirikiano baina ya wafanyakazi ni muhimu. Hata hivyo, kuendesha mambo ya kitengo cha aina hiyo huhitaji meneja ambaye anaweza kuratibu kazi.

Mojawapo ya kitengo muhimu sana cha jamii ni familia; Kuendesha mambo ya kitengo hiki ni jambo la lazima na gumu.

Bila shaka, lazima pawepo na uelewano wa kina sana, na ushirikiano baina ya watu wa familia, lakini pia lazima pawepo kiongozi ambaye anaweza kuwajibika kwa ukamilifu kuhusu mambo ya familia. Ni wazi kwamba, kama familia haimfurahikii mtu anayeweza kuwapanga wengine, itapata usumbufu wa vurugu na ghasia.

Hivyo ama mume lazima awe kama mkurugenzi na mke awe chini yake au kinyume chake.

Hata hivyo, kwa kuwa kipengele cha mantiki ya wanaume kinatawala kipengele cha hisia za wanawake, wanaume wanaweza kuwa viongozi bora zaidi.

Mwenyezi Mungu Mweza wa yote anasema kwenye Qurani Tukufu:


الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنْفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ ۚ فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِلْغَیْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّهُ

 

“Wanamume ni wasimamizi wa wanawake, kwa kufadhiliwa na Mwenyezi Mungu baadhi yao juu ya baadhi, na kwa mali yao wanayotoa. Basi wanawake wema ni wale wenye kutii ….” (Quran 4:34).

Hivyo, ni kwa manufaa ya jamaa wa familia kumheshimu mwanaume kama mlinzi wao na mkuu wao, na kutaka usimamizi wao katika matendo yao.

Hata hivyo, mtu asihitimishe kwamba hadhi ya mwanamke ndani ya nyumba inadunishwa, lakini ni kweli kwamba kudumisha utaratibu na nidhamu ndani ya nyumba ni majukumu yanayohitaji utendaji wa mume. Wanawake wanaoweza kufikiri bila upendeleo, wanaweza kuthibitisha tendo hili.

Mwanamke alisema: “Tulikuwa na desturi nzuri Iran ambayo kwa bahati mbaya imefifia pole pole. Kwenye mila hii mwanaume alikuwa ndiye mkuu wa mambo ya familia. Alikuwa ndiye msimamizi. Siku hizi hata hivyo hali imebadilika na familia haziwezi kufanya uamuzi kuhusu nani awe mkuu.

Ninaamini kwamba mwanamke wa leo, ambaye kwa namna moja au nyingine anayo hadhi sawa na ya mwanaume katika jamii, anaweza kukubali mume wake kama mkuu wa kaya…Desturi hii ya zamani inatakiwa ipendekezwe kwa mwanamke kijana wa leo, ambaye anayo nia ya kuolewa.

Anatakiwa kuingia nyumbani kwa mumewe akiwa amevaa vazi la harusi na kutoka ndani ya nyumba hiyo akiwa amevaa sanda.”

Ni kweli kwamba shughuli za maisha ya kila siku hazimruhusu mwanaume kushiriki katika mambo yote ya familia na kwamba kwa kawaida mke ndiye anaye endesha familia kufuatana na atakavyo, lakini hata hivyo haki ya kuamuru hubaki kwa mwanaume, na kwa hali hiyo lazima ahishimiwe.

Kwa hiyo, inapotokea mwanaume kutoa maoni yake kuhusu jambo lolote la familia au anashauri kitu chochote, mke hatakiwi kumpinga au kumnyima mume wake haki yake kuamuru kwa namna yoyote ile. Vinginevyo, mwanaume atajifikiria yeye hana mamlaka na kumuona mke wake kama mwanamke asiye na adabu na shukrani. Mwanaume anaweza kujenga kinyongo dhidi yake na katika hatua ya baadaye, anaweza hata kukataa matakwa ya halali ya mkewe.

Mtume (s.a.w.w) wa Mwenyezi Mungu alisema: “Mwanamke mzuri atajali matakwa ya mumewe, na atafanya kwa mujibu wa apendavyo mumewe.”

Mwanamke alimuuliza Mtume (s.a.w): “Mwanamke anawajibu gani kwa mume wake?” Mtume (s.a.w.w) alisema: “Mwanamke lazima amtii mume wake na asikiuke amri zake.”

Mtume (s.a.w.w) pia alisema: “Mwanamke mbaya sana miongoni mwa wanawake ni yule ambaye ni mkaidi na sugu.”

Mtume (s.a.w.w) pia alismema: “Mwanamke mbaya zaidi miongoni mwa wanawake ni yule ambaye ni mgumba, mchafu, sugu na asiye mtiifu.”

Bibi mpendwa! Kubali mamlaka ya mume wako. Taka usimamizi wake kuhusu mambo yenu ya familia. Usikiuke amri zake. Usikatae au kuweka pingamizi, yeye hushiriki katika mambo ya nyumbani na familia. Usikatae kushiriki kwake hata kwenye yale mambo ambayo wewe una utaalamu nayo. Usifanye vitendo vya kuonesha kwamba yeye hana mamlaka.

Mruhusu ashiriki katika kazi zako mara chache. Wafundishe watoto wenu kuhishimu mamlaka yake na waambie lazima waombe ruhusa kutoka kwa baba yao kuhusu mambo yao. Watoto wenu lazima watambue kwamba hawatakiwi kukiuka amri zake tangu utoto wao.

Kwa njia hii watoto wenu watakuwa na malezi ya kuwatii wazazi wao.