پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Uwe Na Tabia Njema

Uwe Na Tabia Njema

Dunia huchukua mkondo wake kufuatana na mpangilio linganifu. Matukio hutokea na kujidhihirisha moja baada ya lingine. Kuwepo kwetu katika ulimwengu huu mpana ni kama chembe ndogo ilioko kwenye mwendo na kuathiri chembe nyingine papo hapo.

Uendeshaji wa dunia huu haupo katika uwezo wetu na matukio ya dunia hii hayatokei kufuatana na utashi wetu. Tangu hapo ambapo mtu hutoka nyumbani kwake asubuhi hadi hapo anaporudi jioni, inawezekana hukabiliana na mamia ya mambo yasiyofurahisha.

Mtu hukutana na matatizo mengi sana katika uwanja wa maisha. Inawezekana mtu akakutukana, na mfanyakazi mwenzake asiye rafiki, utangojea basi kwa muda mrefu mno, umeshutumiwa kwa sababu ya kitu fulani ofisini, umepoteza fedha, au umekabiliwa na tukio lolote ambalo linaweza kumtokea mtu mwingine yeyote popote.

Inawezekana ukakasirishwa sana na matukio ya kawaida ya kila siku katika maisha yako hivyo kwamba unafanana na bomu lililotegwa na kulipuka wakati wowote.

Vema, inawezekana ukadhani kwamba huwezi kuwalaumu watu wengine au dunia kwa sababu ya bahati yako mbaya, hivyo kwamba unaporudi nyumbani, unajaribu kutoa nje hasira yako kwa mke wako na watoto wako.

Unaingia nyumbani kwako kama vile ‘Ziraili’ (malaika wa kifo) amewasili. Watoto hutawanyika kama panya wadogo mbele yako. Mungu na apishe mbali kwamba uone kitu fulani kilicho kosewa! Chakula, ama inawezekana kina chumvi nyingi au hakina chumvi, au kikombe chako cha chai hakijawa tayari, inaewezekana nyumba chafu, au watoto wanapiga kelele na kwa hiyo unapata kisingizio cha kulipuka kwa hasira ndani ya nyumba yako.

Halafu unamkasirikia na kumpigia kelele kila mtu, unawatukana unawapiga watoto na kadhalika. Wakati huo utakuwa umeigeuza nyumba ya huba na urafiki kuwa jahanamu iwakayo moto ambamo wewe na familia yako mtateseka.

Kama watoto wanaweza kukimbia kutoka nyumbani na kwenda mitaani, watafanya hivyo, na kama hawawezi kufanya hivyo, basi watahesabu sekunde hadi hapo utakapoondoka nyumbani.

Inaeleweka dhahiri ni mazingira ya kusikitisha na kutisha yalioje yanayotawala familia za aina hii. Kila mara upo ugomvi na mabishano. Nyumba yao kila mara imevurugika. Mke anachukia kuona uso wa mume wake.

Mwanamke anawezaje kuishi kwa furaha na mwanamume mkali na mwenye hasira?

Baya zaidi kuliko yote ni hatima ya watoto ambao watakulia kwenye mazingira hayo. Ugomvi wa wazazi wao kwa hakika utatia kovu kwenye roho na nyoyo zao zilizo nyepesi kuhisi. Watoto wanao wanaopata matatizo kama haya huendeleza tabia ya kuwa aina ya watu wenye hasira, wagomvi wenye huzuni na kuona kila jambo ni baya wakati watakapofika umri a utu uzima. Hukatishwa tamaa kwenye familia yao na hukengeuka. Inawezekana wakakutana na mitego ya watu waovu na kuanza kufanya uhalifu wa aina mbali mbali. Inawezekana wakawa na tabia ngumu sana kuelezeka na kuvurugikiwa akili hivyo kwamba wanaweza kuhatarisha maisha ya watu wengine kwa kuua au kujiua.

Msomaji anashauriwa kufanya utafiti wa historia ya maisha ya wahalifu. Takwimu na taarifa za kila siku za matukio ya uhalifu yote yanaonesha ukweli huu.

Yote haya yapo kwenye wajibu wa mlezi wa familia ambaye ameshindwa kudhibiti tabia yake na ameitendea vibaya familia yake. Mtu kama huyu kamwe hawezi kuwa na amani katika dunia hii na ataadhibiwa akhera.

Mpendwa bwana! Hatuna nafasi na hatuwezi kudhibiti mambo ya dunia hii. Mabalaa, shida, na matukio ya kusikitisha yote ni mambo yanayo ambatana na maisha haya. Kila mtu hupata matatizo wakati mbali mbali. Ni ukweli wa mambo kwamba, mtu hufika kwenye umri wa balekhe kwa kukabiliana na taabu. Mtu lazima apambane nayo kwa nguvu na lazima ajaribu kutafuta ufumbuzi wake. Binadamu wanao uwezo wa kukabiliana na mamia na matatizo madogo na makubwa na bila kukata tamaa chini ya mbinyo wa balaa.

Matukio ya dunia si ndio tu sababu ya kutibuliwa kwetu, isipokuwa hasa zaidi ni mpangilio wetu wa neva ambao huathirika na matukio kama haya na husababisha sisi tukose furaha. Kwa hiyo, kama mtu angeweza kudhibiti hali wakati anapokabiliwa na matukio ya maisha yasiyofurahisha, hangekasirika na kuchukia.

Tudhani ya kwamba umepatwa na tukio lisilofurahisha. Tukio hili ama ni matukio ya kila siku yalioambatana na hali ambayo hatuna uwezo wa kuingilia au hatuwezi kusaidia. Au inawezekana tukio hili ni lile ambalo sisi tunaweza kufanya uamuzi wetu.

Ni dhahiri kwamba katika mfano wa kwanza, hasira yetu hainge saidia kwa njia yoyote. Tutakuwa tunakosea kukasirika au kuhamaki. Lazima tukumbuke kwamba sisi hatukusababisha kutokea kwa tukio hilo na hata tujaribu kulikaribisha kwa uso wenye furaha.

Lakini kama tatizo letu ni la mfano wa pili, basi tunaweza kutafuta ufumbuzi unaofaa.

Kama hatutakata tamaa tunapokabiliwa na shida na kujaribu kujizuia, kwa kutumia busara, tunaweza kuyashinda matatizo yetu. Kwa njia hii hatuta kimbilia hasira ambayo inaweza kuwa tatizo juu ya tatizo.

Tunao uwezo wa kushinda matatizo yote kwa kutumia uvumilizu na hekima. Hivi si jambo la kusikitisha kwamba tunashindwa kudhibiti mambo yanayotokana na matukio yasioepukika maisha?

Zaidi ya haya kwa nini umlaumu mke na watoto wako kwa mabalaa yako? Mke wako anatekeleza mgawo wa wajibu wake. Anatakiwa kutunza nyumba na watoto. Anatakiwa kufua, kupika, kunyoosha pasi kufanya usafi na kadhalika. Unatakiwa kumtia moyo mke wako kama vile unavyomtendea.

Watoto wako pia wanafanya kazi yao. Wao pia wanamngojea baba yao wajifurahishe. Wafundishe mambo yaliyo sahihi na uwape hamasa wajifunze zaidi. Je, ni haki kwamba unakutana na familia yako ukiwa na uso wa kikatili na chuki?

Wanakutarajia wewe kuwatimizia matakwa ambayo ni haki yao. Wanatazamia wema kutoka kwako na wanataka uzungumze nao kwa upole na uoneshe furaha.

Watakuchukia sana kama ukidharau hisia zao na kama utaigeuza nyumba kuwa mahali pa giza ambamo hakuna furaha hata kidogo.

Unajua watateseka kiasi gani kutokana na tabia yako isiyopendeza na ya kikatili? Hata kama hutaichukulia familia yako kwa uzito uanostahili angalau ujihurumie wewe mwenyewe. Uwe na uhakika kwamba unaweza kuharibu afya yako kwa kuendeleza ukali.

Unawezaje kuendelea kufanya kazi na unawezaje kufuzu kupata mafanikio? Kwa nini uigeuze nyumba yako iwe jahannamu? Hivi si vizuri zaidi kwamba wewe uwe na furaha kila mara na uyakubali matatizo yako kwa busara na si hasira?

Hungetaka kuamini kwamba hasira haiwezekani kutatua matatizo yako, isipokuwa hasa zaidi matatizo yataongezeka? Hungekubali kwamba unapokuwa nyumbani unatakiwa kupumzika na kurudisha nguvu zako ili uweze kupata ufumbuzi unaofaa kwa matatizo yako akili yako ikiwa imetulia? Kutana na familia yako ukiwa na uso wenye tabasamu; taniana na watu wa familia yako kwa namna nzuri na jaribu kutengeneza mazingira ya furaha nyumbani kwako. Ule na kunywa pamoja nao na upumzike.

Kwa njia hii wewe na familia yako mtafurahia maisha na mtashinda matatizo yenu kwa urahisi. Ndio sababu dini tukufu ya Uislamu inaona tabia njema kuwa sehemu ya dini na ishara ya kiwango cha juu sana cha imani.

Mtume (s.a.w) alisema: “Mtu mwenye tabia njema amekamilika zaidi katika imani yake. Mtu mwema zaidi miongoni mwenu ni yule anayeitendea mema familia yake.”

Mtume (s.a.w) pia alisema: “Hakuna tendo jema zaidi kuliko tabia njema.”

Imamu Sadiq (a.s) alisema: “Kuwatendea wema watu na kuwa na tabia inayostahili unapokuwa nao kufanya miji huwa na watu wengi zaidi na umri wa raia huongezeka.”

Imamu Sadiq (a.s) pia alisema: “mtu muovu hubakia kwenye mateso na uchungu.”

Luqman mwenye hekima alisema: “Mtu mwenye busara lazima afanye mambo kama mtoto mdogo wakati anapokuwa na familia yake, na kuendelea na tabia ya kiwanamume anapokuwa nje ya nyumba yake.”

Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alisema: “Hakuna furaha iliyo nzuri zaidi kuliko tabia njema.”

Mtume (s.a.w.w) pia alisema: “Tabia njema ni nusu ya dini ya Uislamu.”

Imesimuliwa kwamba alipokufa Sad bin Maadh mmojawapo wa sahaba mashuhuri wa Mtukufu Mtume (s.a.w), Mtume (s.a.w) alishiriki kwenye maziko yake bila kuvaa viatu, kama vile alipoteza mmojawapo wa watu wa familia yake.

Mtume (s.a.w) aliweka maiti ya sahaba huyo karibuni kwa mikono yake iliyotakasika halafu akaufunika. Mama yake Sad ambaye alikuwa anaangalia heshima ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kwa mwanae alimwambia Sad: “Ewe Sad! furahia Pepo” Mtume (s.a.w.w) alimwambia:

“Ewe mama wa Sad, usiseme hivyo, kwa sababu Sad sasa hivi amepata mateso kwa njia ya kugandamizwa kaburini na kadhalika. Baadaye, Mtume (s.a.w.w) alipoulizwa kuhusu sababu ya mateso ya Sad, Mtume (s.a.w.w) alijibu; “Ilikuwa kwa sababu alikuwa anaitendea mabaya familia yake.”