پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Mtunze Mke Wako

Mtunze Mke Wako

Mume na mke kila mara huhitaji ushirikiano wa kila mmoja wao na kuonesha mapenzi kwa kila mmoja. Hata hivyo, haja hili huwa kubwa zaidi wakati wa ugonjwa na matukio mengine yanayo fanana na hilo. Mtu mgonjwa, kama vile anavyohitaji daktari na dawa, huhitaji matunzo na uangalizi wenye mapenzi. Muuguzi mzuri humsaidia mgonjwa kupona vizuri na haraka.

Mwanamke pia hutegemea mume wake kumtunza yeye wakati anaugua na kulala kitandani. Mke anatarajia mume kumtunza yeye zaidi ya wazazi wake.

Mwanamke anaye fanya kazi nyumbani kama mtumishi wa nyumbani anastahili uangalizi ulio na mapenzi kutoka kwa mume wake. Anatarajia kwamba ni haki yake mume wake amuuguze.

Malipo ya tiba na dawa ni mojawapo ya matumizi ya kawaida ya maisha na mwanaume anao wajibu wa kumpa fedha hizo muhimu. Mwanamke anayefanya kazi nyumbani bila mshahara wowote, hakika anayo haki ya kumtarajia mume wake kulipa gharama ya tiba yake.

Wapo wanaume ambao hawana aibu kufanya isivyo haki. Huwatumia wake zao wakati wana afya njema na wenye uwezo, lakini hukataa kulipa fedha wanapo ugua. Fedha yoyote ndogo wanayotumia kwa ajili ya tiba ya wake zao huilalamikia sana. Baadhi ya wanaume, wakiona gharama ya tiba ni kubwa wanaweza hata kuwaacha wake zao. Tabia hii ni sawa kweli? Mwanamke mmoja alikuwa analalamika kuhusu mume wake. Alisema: “Nilikuwa nafanya kazi kwa bidii nyumbani na nilipita kwenye nyakati nyingi za furaha na shida na mume wangu. Hata hivyo, sasa nimeugua, mume wangu anataka kuniacha!”

Bwana mpendwa! Kama unapenda kuwa na furaha na maendeleo ya familia yako, lazima umpeleke mkeo kwa daktari anapougua. Lazima ulipe gharama ya matibabu yake. Zaidi ya hapo, lazima umuuguze kwa wema. Sasa amewaacha wazazi wake ili aishi na wewe, anatarajia wewe kuwa na mapenzi zaidi kwake kuliko wazazi wake. Yeye ni mwenzako na mama wa watoto wako! Mhurumie na mpe matumaini ya kupona haraka. Mpikie chakula. Tayarisha chakula kinachofaa na nunua vifaa vilivyoelekezwa. Mlishe chakula. Yote haya yatamfanya mke wako afurahi.

Wanyamazishe watoto. Uwe mwangalifu wakati wa usiku. Wakati wowote akiamka muulize hali yake anavyojisikia. Kama hawezi kulala kwa sababu ya maumivu, basi na wewe uwe macho. Unaweza hata kuwaambia watoto wenu wakusaidie kumwangalia mama yao. Usimwache hata kidogo mke wako bila huduma, hasa zaidi anapokuwa anaumwa. Wakati kama huo, mke wako ataona mapenzi yako na yeye atakupenda zaidi. Atajivuna kwa sababu hiyo na atakuwa tayari kukuhudumia wewe na watoto zaidi, mara atakapo pona.

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Mtu mzuri zaidi miongoni mwenu ni yule ambaye ni mwema zaidi kwa familia yake, na mimi ni mwema kuliko wote kwa familia yangu.”

Mtukufu Mtume (s.a.w.w) wa Uislamu pia alisema: “Yeyote anayefanya jitihada kutambua haja ya mgonjwa, dhambi zake zitasamehewa, na atakuwa kama siku aliyozaliwa.” Mmoja wa maansari (wenyeji wa Madina) aliuliza: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Wazazi wangu na watolewe muhanga kwa ajili yako, ni vipi endapo mgonjwa anatoka miongoni mwa familia yako- Ahlul –bait? Hakuna thawabu nyingi zaidi katika mfano huu?”

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alijibu: “Ndio.”