پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Mpende Mkeo

Mpende Mkeo

Mwanamke ni kituo cha wema na ni kiumbe chenye hisia kubwa sana. Kuwepo kwake hutegemea huruma na upendo. Huwa na shauku ya kupendwa na wengine na jinsi anavyopendwa zaidi ndivyo anavyofurahi zaidi. Hujitolea sana ili apendwe na wengi. Tabia hii ina nguvu sana ndani mwake hivyo kwamba akigundua kwamba hakuna mtu anaye mpenda, basi atajitambua kama ameshindwa. Atakasirika na atahisi kuvunjika moyo.

Kwa hiyo, kwa hakika mtu anaweza kudai kwamba siri ya mwanamume aliyefuzu katika maisha ya furaha ya ndoa ni jinsi anavyo onesha mapenzi kwa mke wake.

Bwana mpendwa! Mke wako kabla ya kuolewa na wewe, alikuwa anafaidi mapenzi ya wazazi wake na wema wa wazazi wake. Sasa ameingia kwenye mkataba wa ndoa na wewe na sasa amechagua kuishi na wewe katika maisha yake yote, anatarajia wewe umtimizie matakwa yake ya mapenzi na huba. Anatazamia wewe kuonyesha mapenzi zaidi kwake kuliko alivyopokea kutoka kwa wazazi wake na marafiki zake. Amekuamini wewe sana na ndio sababu amekupa udhamini wa maisha yake.

Siri ya ndoa yenye furaha hutegemea jinsi unavyodhihirisha mapenzi yako kwa mkeo.

Ukitaka kuuvutia moyo wake, ukitaka awe mtiifu kuhusu matakwa yako kama kuimarisha ndoa yenu, ukitaka mkeo akupende wewe, au adumishe uaminifu kuliko au… basi lazima kila mara uoneshe mapenzi na huba yako kwake.

Usipokuwa mwema kwa mke wako, basi anaweza kupoteza mvuto kwenye nyumba yake, halikadhalika na watoto pia. Na zaidi ya yote kwako wewe mwenyewe. Wakati wote nyumba yako itakuwa katika hali machafuko. Hatakuwa tayari kufanya juhudi kwa ajili ya mtu asiyempenda.

Nyumba ambayo ndani yake haina mapenzi, hufanana na jahanamu inayowaka moto, hata kama ni nadhifu sana na iliyojaa vitu vya anasa.

Mke wako anaweza kuugua au kupatwa na mfadhaiko. Anaweza kutafuta kupendwa na wengine kama hatoshelezwi na wewe. Anaweza asikuthamini wewe na nyumba yako pia, kiasi kwamba anaweza hata kuomba talaka!

Unawajibika kwa yote haya kwa sababu umeshindwa kumtosheleza mkeo. Kwa hakika ni kweli kwamba taratibu zingine za kutalikiana hutokea kwa sababu ya ukatili wa mume au kinyume chake.

Angalia takwimu zifuatazo. Mahitaji ya saikolojia ya mapenzi, uzembe wa waume kuhusu matakwa ya wake zao na kutokuzingatia umuhimu wa hadhi ya kiakili ya wanawake, ni vipengele ambavyo vimekuwa sababu ya kesi nyingi za kutalikiana.

Mnamo mwaka 1969 miongoni mwa kesi za kutengana 10372, katika kesi 1203 wanawake walionesha sababu ya kutaka kutalikiana kuwa ni kuvunjwa moyo kimaisha, kujihisi hathaminiwi na upungufu wa waume kutokujali matakwa na hisia kubwa za wake zao.” 146

Mwanamke alisema mahakamani; “Nipo tayari kuacha mahari yangu na hata kumlipa mume wangu fedha ili akubali kunipa talaka. Mume wangu anawapenda zaidi kasuku wake ndio sababu sitaki kuishi naye zaidi ya sasa.”

Mapenzi na urafiki wa familia ni thamani kubwa zaidi kuliko chochote na ndio sababu Mwenyezi Mungu ameiona hiyo kama mojawapo ya alama za uwezo na neema kubwa ambayo mwanadamu amepewa. Qurani Tukufu inasema:

    وَمِنْ آیَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَکُمْ مِنْ أَنْفُسِکُمْ أَزْوَاجًا لِتَسْکُنُوا إِلَیْهَا وَجَعَلَ بَیْنَکُمْ مَوَدَّةً وَرَحْمَةً ۚ إِنَّ فِی ذَٰلِکَ لَآیَاتٍ لِقَوْمٍ یَتَفَکَّرُونَ

“Na katika ishara zake ni kuwa amekuumbieni wenza kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo ishara kwa watu wanaofikiri (Quran 30:21).”
Imamu Sadiq (a.s) alisema: Yeyote ambaye ni rafiki yetu huonesha wema zaidi kwa mke wake.”

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Jinsi mtu anavyozidi kuwa mwaminifu ndivyo anavyozidi kuonesha wema kwa mke wake.”

Imamu Sadiq (a.s) alisema: “Mmojawapo ya sifa bainifu ya Mitume wa Mwenyezi Mungu ni kwamba wote ni wema kwa wake zao.”

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Maneno ya mwanaume anaye mwambia mke wake; ‘Ninakupenda kweli’ kamwe hayaondoki moyoni mwake.”

Kama mambo yalivyo, mapenzi na huba lazima yawe halisi na kuvutia kwenye moyo wa mwingine, lakini hata kupenda sana kwa mtu haitoshi, kwa kuwa ni muhimu kuonesha huba. Kwa kuonesha hisia zako kwa maneno na vitendo vyako, mapenzi unayoonesha, yatapata jibu zuri kutoka kwa mkeo na nyoyo zenu zitaimarisha muungano wa mapenzi.

Uwe wazi na udhihirishe mapenzi yako kwako bila kusita. Wakati yupo au hayupo, msifie. Mwandikie barua unapokuwa safarini na mtaarifu kwamba kutokuwa karibu naye unajihisi mpweke sana. Mara kwa mara mnunulie kitu kama zawadi. Mpigie simu unapokuwa ofisini au shughuli zako na umuulize hali yake.

Kitu kimoja cha muhimu sana kwenye akili ya mwanamke ni namna hizi za kuonesha mapenzi kwake.

Bibi fulani wakati analia kwa masikitiko alisema. “Niliolewa na mume wangu usiku mmoja wa majira ya kupukutika kwa majani. Tuliishi pamoja kwa amani kwa muda fulani. Nilihisi kuwa nilikuwa mwanamke mwenye bahati kubwa sana hapa duniani. Niliishi kwenye nyumba yake ndogo kwa miaka sita. Nilihisi ninayo furaha mara mia moja nilipogundua kwamba nilikuwa mja mzito.

Nilipomtaarifu mume wangu alidondokwa na chozi la furaha wakati amenikumbatia mikononi mwake. Alilia sana hivyo kwamba karibu angeshindwa kujizuia. Halafu akatoka nje na akaninunulia mkufu wa almasi kwa fedha yake ya akiba. Alinipa mkufu na akasema: ‘Ninatoa hii kwa mwanamke bora kuliko wote ambao ninewaona hapa duniani.’ Lakini baada ya muda mfupi alikufa kwenye ajali ya gari.”