پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Uwe Mwenye Kushukuru

Uwe Mwenye Kushukuru

Kazi ya utunzaji wa nyumba inaweza kuonekana kama kazi rahisi kwa wanaume wengine, lakini itakuwa ni jambo la kuridhisha kukubali kwamba kazi hii ni ngumu na inachosha.

Mama wa nyumbani! Hata kama atafanya mchana kutwa na usiku kucha hataweza kumaliza kazi yake yote.

Kupika kufanya usafi, kufua nguo na kunyosha pasi kuosha vyombo na kuvipanga, kutandika vitanda na kupanga fenicha na zaidi ya yote kuwatunza watoto, si siku moja, lakini, ni kila siku ni ngumu sana.

Mwanaume anaweza kufikiri kwamba mke wake anapika tu mara tatu kwa siku na kusahau kazi zake zingine nyingi sana.

Ni mwanaume huyo tu ambaye atakuwa tayari kukaa nyumbani kwa kipindi cha mwezi moja na afanye kazi ya nyumbani ndiye atajua shinikizo lililopo, na hapo ndipo atakapo pendezwa na juhudi za mke wake.

Mke wa nyumbani hufanya kazi hii yote kwa furaha lakini hutarajia mume wake kupendezwa naye na kuonesha shukrani zake.

Bwana mpendwa! Kuna ubaya gani ukimpa ahsante mke wako kwa kazi ya kutunza nyumba? Kwa nini usioneshe upendo kwa chakula anachopika? Kuna ubaya gani ukimshukuru mke wako kuhusu juhudi zake za kutunza watoto? Hutambui kwamba kupendezwa kwako kwa jitihada zake ni kitendo cha kumtia moyo na kumchangamsha?

Kama hutajali jitihada zake, au hutaki kumshukuru atapoteza mvuto wa kazi ya kutunza nyumba na halafu wewe utalalamika. Lazima utambue kwamba wewe unaweza kuwa chanzo cha uvivu wa mkeo.

Kama mgeni anakupa upendeleo mdogo, ungemshukuru mara nyingi sana, lakini mke wako anayekupendelea mara nyingi, humshukuru hata mara moja! Wewe haupo tayari kumfurahia kwa kuonesha kupendezwa kwako kwa jitihada zake zote.

Mama wa nyumbani mwenye umri wa miaka ishirini na tisa aliandika kutoka Tehran. “Nimeolewa na mwanaume asiye na shukrani na asiye pendezwa ambaye hajali kabisa kazi yangu ya kutunza nyumba. Ninafua, ninafanya usafi, ninapika, ninapamba nyumba, ninafuma sweta kwa ajili ya familia, hupiga rangi viatu vyake, hupiga pasi nguo zake na kadhalika na hajawahi kunishukuru hata mara moja. Wakati wowote ninapomwambia kuhusu kazi za nyumbani huingilia kati na kusema kwamba nisisifie kazi hiyo mbele yake. Anadharau juhudi zangu, ambapo kufaulu kwake kunategemea sana bidii yangu.”

Baadhi ya wanaume hufikiri ni kitendo cha ujasiri wa kiume kutojali kazi za nyumbani za wake zao. Wanadhani kama wakitoa pongezi kwa kazi hiyo ya wake zao, wanawake wataharibika. Wanaweza hata kuamini kwamba mume na mke hawahitaji kupeana ahsante wao kwa wao.

Imani hii si sahihi, kwa sababu yeyote anaye tenda wema kutoka katika mtizamo wa kisaikolojia anahitaji kupewa shukrani na kuthaminiwa.

Kufurahia jambo la mtu humpa hamasa ya kufanya vizuri na hii ni kweli hususan kwa mama wa nyumbani ambaye hufanya kazi ya kuchosha kila siku tena na tena.

Hivyo Uislamu unaona kitendo cha kutoa shukrani ni sifa njema katika tabia ya mtu. Imamu Sadiq (a.s) alisema: “Yeyote anayemsifu Mwislamu, Mwenyezi Mungu humwandikia sifa nyingi hadi Siku ya Hukumu.”

Mtume (s.a.w.w) wa Uislamu alisema:

“Yeyote anayemheshimu Mwislamu, na kusema naye kwa uchangamfu, na humwondoshea huzuni, wakati wote atakuwa kwenye neema za Mwenyezi Mungu.”